Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kushiriki mapambano dhidi ya COVID-19

June 29, 2020

Kwa miaka 12, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeasisi na kutekeleza tafiti na programu mbalimbali zinazohusiana na magonjwa ambukizi kwa kutumia dhana ya Afya Moja. Katika kutekeleza azma hii, Chuo kinashirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, Wakala wa Maabara ya Veterinari na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori. 

Programu hizo zimekuwa zikiratibiwa na Taasisi ya Afya Moja ya SACIDS (SACIDS Foundation for One Health). Lengo kuu la SACIDS ni kujenga uwezo wa nchi za Kusini mwa Afrika kukabiliana na magonjwa ambukizi ya binadamu na wanyama. 

Kituo hiki kinaungana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kutoa utaalamu wa kuzuia na kudhibiti magonjwa ambukizi na hasa mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19). 

SACIDS ilibaini hatari ya ugonjwa COVID-19 kuenea hadi Bara la Afrika, ikiwemo pia Tanzania, baada ya tarifa za kuwepo kwa COVID-19 nchini China na Bara la Ulaya mapema Februari 2020. Kufuatia kuwepo kwa mlipuko wa COVID-19 katika maeneo mbalimbali duniani, SUA, kupitia SACIDS kiliwasilisha andiko kwa Skoll Foundation na kufanikiwa kupata ufadhili wa kuboresha utaalamu wa kukabiliana na dharura ya COVID-19 nchini Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji na Zambia. 

Kupitia mpango huo, SUA inatoa utaalamu katika maeneo yafuatayo: 

i. Uchunguzi wa kimaabara ikiwa pamoja na uainishaji wa vinasaba vya vimelea vya COVID-19; 

ii. Teknolojia na sayansi katika saveilensi hususani katika maeneo ya viwanja vya ndege na mipaka ya nchi kavu/majini; pamoja na ufuatiliaji wa matukio ya maambukizi katika jamii; 

iii. Mafunzo kwa wataalamu wa maabara na saveilensi; na 

iv. Tathmini ya uwepo wa hatari ya COVID-19 na uwezo wa kupambana nayo. 

Baada ya kubainika kuwa COVID-19 imeingia Barani Afrika katika nchi za Misri na Afrika Kusini, SUA kwa kushirikiana na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ilifanya maandalizi ya kujenga uwezo wa maabara hiyo kupima COVID-19. Nia ilikuwa ni kuandaa mazingira ya kuwezesha upimaji wa maambukizi ya COVID-19 hapa nchini. 

Halikadhalika, SACIDS kinashirikiana na maabara hiyo ya taifa katika kuchambua vinasaba vya virusi Corona. Teknolojia ya uchambuzi wa vinasaba inayotumika imewahi kutumiwa na SUA katika kuchambua virusi vinavyosababisha Homa ya Nguruwe na Sotoka ya Mbuzi na Kondoo. 

Matumizi ya teknolojia hii yatawezesha kubaini matabaka ya virusi vya Corona na kuoanisha matabaka hayo na athari za kiafya kwa wagonjwa wa COVID-19. Uelewa wa vinasaba vya virusi vya Corona utasaidia katika kufahamu matabaka ya virusi vinavyosambaa nchini na iwapo virusi hivi vitaweza kukingwa na chanjo zitakazotengenezwa. Halikadhalika, mpangilio wa vinasaba wa virusi vya Corona utaweza kuonyesha iwapo kuna mabadiliko na yataathiri vipi hali za wagonjwa. 

SUA imebuni programu ya simu za mkononi (AfyaData) inayoweza kutumiwa na wahudumu wa afya kufanya saveilansi kuanzia ngazi ya jamii, zahanati hadi hospitali za rufaa. Programu hii inaweza kutumika kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili, 

Kiingereza na lugha nyinginezo; inaruhusu wataalamu wa afya kutoa mafunzo na mrejesho kwa wahudumu wa ngazi zote. Hali kadhalika, wataalamu wetu wanatengeneza moduli maalum kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya kukusanya na kuchakata taarifa za wasafiri katika maeneo ya bandari, viwanja vya ndege na mipaka ya nchi. 

 

SOURCE: Ministry of Education Tanzania www.moe.go.tz

Share on FacebookTweet about this on TwitterShare on LinkedInShare on Google+Email this to someone